Dec 12 2011
CCM yamgeuka Spika posho za wabunge
Spika wa Bunge Anne Makinda
SASA YATAKA WABUNGE WAKE KUZIKATAA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hatimaye kimepinga uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, wa kuongeza posho za vikao kwa wabunge na kimewataka wabunge wa chama hicho kuziacha.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, imesema sababu za kuongezeka kwa posho za wabunge kama zilivyotolewa na Spika Makinda, hazilengi kutatua tatizo, badala yake zitazua matabaka na kuongeza pengo kati ya walionacho na wasio nacho.
CCM kimesema kuwa suala la kupanda kwa gharama za maisha haliko Dodoma wala kwa wabunge peke yao, bali ni la nchi nzima na ndiyo maana nyongeza hizo zimeibua mjadala mkubwa miongoni wa wananchi wa kawaida, wanaharakati, wasomi na wanasiasa, waliodai kuwa nyongeza hizo ni ufujaji wa fedha wakati huu ambapo makundi ya watumishi wengine wamekuwa wakidai kulipwa mafao yao na serikali bila mafanikio.
“Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia 200, kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000. Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha Bunge kwa siku. CCM kimefuatilia kwa makini suala hilo na kutolea msimamo wake,” alisema Nape.
Nape alisema kuwa linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo kwa makundi yote katika jamii na si kwa wachache ndani ya jamii.
“Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo inasababisha hofu na mashaka miongoni mwa Watanzania,” alisema Nape.
Katibu huyo aliongeza kuwa swali kubwa kwa Watanzania hao ni je, maisha yanapanda Dodoma peke yake na kwa wabunge tu? Aliongeza kuwa CCM kwa kuzingatia masilahi ya nchi na jamii kwa ujumla, inawataka wabunge wao na mamlaka nyingine zinazohusika na suala la nyongeza za posho kwa wabunge kulitafakari upya jambo hili na kuliacha.
“Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafsiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine, wakiwamo walimu, askari, madaktari na wengineo,” ilisomeka sehemu ya taarifa yake.
CCM imesema kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndio wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.
Desemba 6, mwaka huu, Spika wa Bunge Anne Makinda, aliutangazia umma kuwa posho za vikao vya wabunge zilikuwa zimeongezwa kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 kutokana na kile alichosema kupanda kwa gharama za maisha katika mji wa Dodoma.
Kauli ya Makinda ilipingana na ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, aliyoitoa jana yake, akikanusha taarifa za vyombo vya habari zilizofichua siri ya ongezeko hilo la posho kwa wabunge.
Ongezeko hilo hata hivyo lilipingwa vikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kikaweka msimamo kwa wabunge wake kutopokea nyongeza hiyo ya posho.
Wabunge wengine wa upinzani waliopinga ni pamoja na wa NCCR- Mageuzi, wakati wale wa CUF, TLP na CCM wakiunga mkono.
Source: Tanzania daima


